BUNDI mweusi amezidi kulikumba Kanisa la Moravian
Jimbo la Kusini Magharibi kufuatia mgogoro wa muda mrefu ambapo safari hii
baadhi ya waumini na wachungaji walitaka kufunga ofisi za Jimbo hilo
wakishinikiza kujiuzulu kwa Askofu, Alinikisa Cheyo.
Tukio la kufunga ofisi za Jimbo hilo limetokea leo
majira ya saa 12 asubuhi ambapo baadhi
ya Wachungaji na waumini wa kanisa hilo walifika katika makao makuu ya Jimbo
yaliyoko Jakaranda jijini Mbeya wakiwa na makufuri yao.
Kanisa la Moraviani Tanzania, jimbo la kusini
Magharibi kwa zaidi ya mwaka mmoja limekuwa katika mgogoro wa kiuongozi, baada
ya kamati tendaji (KTM-JKM) kumsimamisha Mwenyekiti aliyechaguliwa kihalali
kupitia mkutano Mkuu (Sinod), Nosigwe Buya kwa madai ya kushindwa kulisimamia
kanisa na kumpandisha aliyekuwa Makamu wake, Zacharia Sichone, jambo lililoibua
mpasuko.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigalla King
ndiye aliyenusuru kufungwa kwa kanisa hilo
baada ya kuwasihi wachungaji na Waumini wenye jazba kuwa na subira
wakati Serikali ikijaribu kuona namna ya kutatua mgogoro huo.
Akizungumza na kundi hilo, Mkuu wa Wilaya, Dk.
Sigalla aliyefika eneo hilo majira ya saa 3:20 aliwaomba wachungaji hao,
kusitisha azima yao hiyo ya kuzifunga ofisi za Makao Makuu ya kanisa na kuwa na
subira kwani siku inayofuata serikali
ingetoa msimamo juu ya mgogoro huo.
Akizungumza baada ya kukubali ombi la Mkuu wa
Wilaya, mmoja wa wachungaji hao, Edward Chilale, alisema wamefika hatua hiyo
baada ya Askofu Mkuu wa kanisa hilo,kupuuza madai yao ya kutaka kuitishwa kwa
Mkutano Mkuu wa kanisa (Sinod) utakaoamua hatima ya mgogoro baada ya
kusimamishwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa jimbo hilo, Mwenyekiti Buya.
Mchungaji Chilale alisema licha ya kuheshimu kauli
ya serikali ya kutaka kusitisha mpango wao wa kulifunga kanisa, bado shinikizo
lao la kutaka Askofu Cheyo kujiuzulu bado liko palepale, kwani yeye ndio chanzo
cha yote.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti jimbo hilo,
Sichone, alisema kuwa amesikitishwa na kitendo kilichofanywa na kundi hilo
ndani ya kanisa kwa kuwa kimeenda tofauti na taratibu za kanisa, ambapo mambo
yote hufanywa kupitia vikao.
Alisema tayari wametoa taarifa jeshi la polisi na
kwamba tukio hilo liliongozwa na wachungaji sita wa ushirika wa Bethlehemu
ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiendesha mambo kinyume na taratibu za kanisa.
Wachungaji hao pamoja na kukubali kufungua ofisi
waliweka misimamo yao ambayo Miongoni mwa maazimio hayo ni kuutaka uongozi huo
wa kanisa kubatilisha mara moja maamuzi yake ya kumsimamisha kazi Mwenyekiti
huyo na asibughudhiwe hadi Mkutano Mkuu wa Sinodi.
Pia waliitaka halmashauri kuu iwe imeitisha Mkutano
Mkuu wa Sinodi Machi 3 mwaka huu na kwamba isipotii maazimio hayo ya
wakristo watachukua hatua ya kuzifunga ofisi zote za jimbo na kufanya
maandamano ya amani kwa kibali cha vyombo vya dola.
|
Post a Comment
Post a Comment