Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa
WAKATI mjadala wa kihistoria wa kuunda Katiba mpya ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, ukiwa katika hatua ya kupata kanuni za Bunge
Maalumu la Katiba, baadhi ya wajumbe wameamua kuelekeza nguvu kudai
posho nono.
Wajumbe hao wanapinga posho ya sasa ya Sh 300,000 kwa siku, ambayo
kwa wananchi wa kawaida inaonekana ni kubwa, lakini vielelezo vyao ni
taarifa, kwamba wajumbe ambao wanatoka Baraza la Wawakilishi, wanalipwa
zaidi ya hapo.
Mbali na hoja hiyo ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, ambayo sasa
wajumbe ambao ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wanafikiria
kumbana Spika Anne Makinda, ili nao waongezwe posho kama wenzao wa
Zanzibar, hoja nyingine imetajwa kuwa ni hadhi ya wabunge kwamba
haifanani na Sh 300,000.
Aliyeanzisha hoja hiyo jana ni Richard Ndassa, Mbunge wa Sumve,
ambaye mbali na kutaka nyongeza ya posho, alipinga utaratibu wa kusaini
asubuhi na jioni kwa ajili ya posho zinazotolewa ‘rejareja’,
akipendekeza waaminiwe na walipwe fedha nyingi kwa mkupuo.
Mjumbe mwingine, Suleiman Nchambi, alimwunga mkono Ndassa, lakini
akahoji iweje wajumbe wa Tume ya Kurekebisha Katiba walipwe posho kubwa
nao walipwe kidogo.
Mezani kwa Serikali
Kutokana na hoja hizo, Mwenyekiti wa muda wa Bunge, Pandu Ameir
Kificho, alisema suala hilo linachukuliwa kwa umuhimu na watazungumza na
Serikali liamuliwe baadaye.
“Kuhusu masuala ya posho, kama nilivyosema tunalichukua ili tuangalie
uwezekano wa kuzungumza na Serikali, hili tutaamua hapo baadaye,”
alisema Kificho.
Tume Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge,
Ndassa alisema wajumbe wa Tume walikuwa wakilipwa Sh 500,000 kwa siku
huku madereva wakilipwa Sh 220,000.
“Mimi ninayehangaika kuanzia asubuhi na mimi nalipwa Sh 220,000? Mimi
mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na dereva wa Tume ni sawa?” Alihoji
Ndassa.
Katika Sh 300,000 kwa siku, Sh 80,000 ndiyo posho ya kujikimu ambayo
wajumbe wa Bunge la Katiba watapewa kila siku, iwe amefanya kazi au la,
na Sh 220,000 ni posho ya kazi, ambayo itatolewa kwa waliofanya kazi tu.
Hadhi ya Mbunge “Mimi kwenye hizi laki tatu (Sh 300,000) zangu zote,
ni pamoja na dereva wangu, simu, chakula, mafuta, lakini pia unamtaka
mbunge eti lazima asaini kwanza!” Alionesha mshangao.
Bila kupendekeza kiwango cha kulipwa, Ndassa alitoa mchanganuo wa
matumizi ya mbunge, akisema hoteli ya hadhi yake ni Sh 70,000 kwa usiku
mmoja.
Mbali na gharama hiyo ya malazi, alisema gharama za chakula, mafuta
ya gari, dereva na msaada atakaotakiwa kutoa kwa watu mbalimbali Sh
80,000 haitoshi.
“Hoja yangu ya msingi, ni kwamba Serikali ijaribu kuangalia suala
hili kwa upana, tukiliacha hivi hivi linaweza kuleta tatizo,” alisema
Ndassa.
Kususa
Ndassa alisema wabunge wengine ni wafanyabiashara ambao hawawezi
kukubali kukaa bungeni kwa muda wote wakilipwa posho ya Sh 300,000.
Alipohojiwa anatarajia mtazamo gani kutoka kwa wananchi wanaoishi kwa
kipato cha chini ya dola moja kwa siku (Sh 1,600), huku yeye akikataa
Sh 300,000 kwa siku, Ndassa alisema: “Ukiweka matarajio ya jamii
itasemaje, huwezi kufanya kazi. Maswali kama hayo huwezi kuyakwepa,
binadamu hamwezi kulingana nyote duniani, hata vidole viko tofauti.”
Nchambi alisema kwa upande wao, wabunge hawana tatizo isipokuwa
anatetea wajumbe wengine ambao hawalipwi kiinua mgongo wala mshahara.
“Mbunge anatakiwa alale kwenye hoteli ya angalau Sh 70,000. Hata
wananchi wanatakiwa waelewe kwamba wabunge wamekuja kufanyia kazi Katiba
ambayo ndiyo msingi wao,” alisema Nchambi.
Ubaguzi
Suala lingine lililoibuliwa na Ndassa nje ya ukumbi, ni kuhusu
tofauti ya kiasi cha posho kwa alichosema wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi, wameongezwa Zanzibar wakati wengine wakipokea Sh 300,000.
Bila kutaja kiasi kilichoongezwa, Ndassa alisema:“Lakini wenzetu
Wazanzibari wameongezwa na Baraza la Wawakilishi, wote ni wajumbe wa
Bunge hilohilo… lazima kutakuwa na mgawanyiko. Na sisi tukisema hawa
wabunge wamekwenda kwao wameongezwa na sisi tumwambie Makinda atuongeze,
hawa makundi maalumu watakwenda kuongezwa wapi?
“Kwa kufanya hivyo umeshaweka mgawanyiko inatakiwa tuwe kitu kimoja,
kama ni Sh 20 wote tupewe Sh 20, kama ni Sh 800 wote tuwe sawa,” alisema
Ndassa.
Mwandishi wa habari hizi hakufanikiwa kumpata Katibu wa Baraza la
Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad kufafanua hilo kutokana na kuwa kwenye
kikao.
Lakini taarifa kutoka kwa baadhi ya watendaji wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ), zilithibitisha kwamba wawakilishi waliomba
waongezwe Sh 500,000 lakini hawakupewa zote; wamepewa chini ya hapo.
“Si kweli (hawapokei Sh 420,000) lakini waliomba Sh 500,000 ila
hawakupewa hizo, wamepewa chini ya hapo,” alisema mtoa habari ambaye
hakusema ni kiasi walichoongezwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Utaratibu
Kwa mujibu wa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, wabunge hao
wameshapewa posho ya kujikimu ya Sh 80,000 kwa siku kuanzia Februari 16
hadi 28.
Aliongeza kuwa posho maalumu ya kazi ya Sh 220,000 kwa siku, ambayo
hupigiwa hesabu kutokana na ushiriki wa mjumbe kusaini mahudhurio kila
siku asubuhi na jioni, itakuwa ikiingizwa kwenye akaunti za wajumbe kila
baada ya wiki moja ya kazi.
Na Habari leo
Lumemo blog
Post a Comment
Post a Comment