SHIRIKA la IMARISHA linalofadhiliwa na
Watu wa Marekani limetoa msaada wa Vyombo vya kisasa kwa Kikundi cha Huduma
Majumbani Mkoani Mbeya(KIHUMBE) wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 410
kwa lengo la kuendeleza fani ya ufundi kwa vijana wanaoishi katika mazingira
hatarishi.
Wakizungumza katika Hafla ya
kuwatambulisha wakazi wa Eneo la Sinde A kuhusu umuhimu wa kuwatumia mafundi
walijifunza na kujipatia uzoefu wa kutumia vifaa vya kisasa, Mkurugenzi wa
Mradi wa Imarisha na Kihukbe, Ptolemy Samweli, na Meneja mradi, Tuli Mtatiro,
walisema walilazimika kuomba msaada wa vifaa hivyo baada ya kufanya utafiti
kuhusu upatikanaji wa ajira za mafundi.
Walisema kwa kusaidiana na shirika la
Imarisha , Kihumbe iliona kuna tatizo la kwamba vijana wanaomaliza mafunzo ya
ufundi hawapati ajira na kuamua kufanya utafiti ambao waligundua kwamba
makampuni yenye magrreji na mafundi wa Cherehani wanahitaji watu wenye uzoefu
wa angalau mwaka mmoja ndipo wanaweza kuwapatia ajira.
Walisema baada ya kugundua hivyo walifanya
juhudi ya kuomba msaada wa vyombo vya kisasa kwa Imarisha ili kuweza kuwasaidia
Vijana kupata uzoefu angalau wa Mwaka mmoja ili kuwarahisishia upatikanaji wa
ajira.
Walisema Kihumbe imejikita zaidi katika
kuwafundisha vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi katika Nyanja za
ufundi wa Magari na ushonaji ambapo hadi sasa kituo hicho kina wanafunzi 60,
ambapo 30 wako katika ufundi wa magari na wengine 30 wakiwa katika ushonaji.
Kwa upande wake Mwalimu wa Fani ya
ufundi wa Magari, Alpha Mhava alisema katika kitengo cha ufundi magari
wamepokea mashine za kisasa zenye thamani ya Shilingi milioni 190 vyenye uwezo
wa kufanya shighuli mbali mbali bila kutumia nguvu.
Alivitaja vitu hivyo kuwa ni pamoja na
Mashine ya kutolea matairi ya gari, mashine ya upepo, mashine ya kubalansia
matairi, mashine ya kuangalia matatizo ya injini ya gari, mashine ya kuangalia
mgandamizo wa injini ya Dizeli na Petroli, mashine za kuchomelea, kuchaji
betri,kujazia upepona jeki za kubebea injini na kusombea.
Naye Mwalimu wa ufundi wa Ushonaji,
Elezia Ngoya alisema wanalishukuru shirika la Imarisha kwa kuwaletea vifaa vya
kisasa vya ushonaji vinavyotumia teknolojia ya kompyuta na umeme kwa madai kuwa
vinaendana na mfumo uliopo wa sasa wa kutumia Digitali.
Alisema katika kitengo chake wamepokea
vifaa zaidi ya 22 vyenye thamani ya shilingi Milioni 220 vikiwemo mashine
za kushonea nguo za aina mbali mbali, Overlock(kumalizia ushonaji), kufuma
mapindo, kushona mapambo mbali mbali, kutoboa matundu mbali mbali ya vifungo,
Pasi ya umeme ya kisasa pamoja na mkasi wa umeme.
|
Post a Comment
Post a Comment