HUYU NI BABA YA MTOTO ALIYEPOTEA
MUUNGANO wa Jamii Tanzania(MUJATA)
umeingilia kati sakata la upotevu wa Mtoto wa Miaka mitano uliotokea Wiki
iliyopita katika Mtaa ya Ghana Mashariki kata ya Ghana Jijini Mbeya na
kuwaagiza waliohusika na kitendo hicho kumrudisha mtoto huyo ndani ya siku tatu.
Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa
Mujata,Chifu Soja Shayo Masoko, alipokuwa akizungumza na mamia ya wakazi wa
Mtaa wa Ghana waliokuwa wamefurika kujua hatma ya upotevu wa Mtoto baada ya
Kamati iliyokuwa imeundwa na Serikali ya Mtaa kuomba msaada kwa Mujata baada ya
wao kutafuta bila mafanikio kwa zaidi ya siku kumi.
Awali akizungumza katika mkutano huo,
Mjumbe wa Kamati ya kufanikisha kupatikana kwa Mtoto, Sam Mwashula alisema
Mtoto aliyefahamika kwa jina la Steven Uswege(5) alipotea Januari 17, Mwaka huu
majira ya saa Tano asubuhi baada ya kwenda dukani kununua pipi akiwa na mwenzie
ambapo yeye hakuweza kurudi hadi sasa.
Alisema juhudi za kutafuta zilianza mara
moja ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kituo cha polisi pamoja na vikao vya mara
kwa mara baina ya Wananchi na Serikali ya Mtaa ili kupeana mbinu mbali mbali za
kufanikisha zoezi hilo lakini hadi Siku kumi zinafika hakuna dalili hali
iliyowalazimu kuomba msaada katika Muungano wa Jamii(MUJATA).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wa Mtaa wa
Ghana Mashariki, Philimon Mwansasu, alisema walilazimika kuomba msaada toka
mujata kutokana na mafanikio yalioneshwa na jamii hiyo katika maeneo mbalimbali
kufanikisha kuibua mambo mengi yaliyojitokeza katika jamii yakiwemo ya upotevu
wa watoto.
Alisema pia kitendo hicho kimetokana na
baadhi ya maoni ya wananchi yaliyotokana na mikutano mbali mbali iliyofanyika
mtaani hapo yenye malengo ya kuhakikisha mtoto anapatikana akiwa mzima ama mfu,
ambapo mawazo ya wananchi wengi walielekeza nguvu zao kwa Mujata.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Mujata, Chifu
Soja, alisema wananchi wanatakiwa kuepukana na imani za kishirikina na kuamini
kwamba mtoto huyo amepotea katika mazingira hayo bali waamini kuwa alipokuwa
ametoka nyumbani alishindwa kurudi nyumbani hivyo amepotea katika mazingira ya
kawaida.
Aidha aliwaomba wananchi kuwa na subira
kwa kile alichosema Muungano wa Jamii umeanza kulifanyia kazi suala hilo tangu
walipopata taarifa ambapo Wajumbe wa Mujata wametawanyika katika Wilaya zote
pamoja na mikoa jirani kuhakikisha mtoto anapatikana kwa wakati ama akiwa mzima
au mfu.
Alisema anatoa siku tatu kwa mtu yoyote
aliyehusika na upotevu wa mtoto huyo kuhakikisha anamrudisha ndani ya siku tatu
la sivyo kitu kibaya kitamkuta ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wataalamu wa
tiba asili, waganga wa kienyeji na wataalamu mbali mbali wakiwemo Machifu
kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Mbeya ambao watafanya tambiko kubwa katika mtaa
huo.
Hata hivyo Chifu huyo aliinua imani za
watu baada ya kumuagiza Mama mzazi wa Mtoto aliyepotea Jesca Stephano kwenda
kununua pipi kama aliyokuwa amenunua mtoto wake katika duka lilelile na
kuichukua kwa madai kuwa itamuongoza katika kumpata mtoto.
|
Post a Comment
Post a Comment