SHAHIDI wa tatu katika Kesi
inayowakabili Maaskari wawili na Raia watatu ya unyang’anyi wa kutumia Siraha,
Pasupuret Sreedhar ambaye ni raia wa India na Mhanga wa tukio hilo ameiambia
Mhakama jinsi washtakiwa walivyofanikiwa kuwateka na kuwapora mali zao.
Akizungumza katika kesi hiyo
huku akiongozwa na Wakili wa upande wa Jamhuri, Basilius Namkambe mbele ya
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, Michael Mteite, Shahidi huyo
ambaye hakuweza kuzungumza Kiswahili kabisa hali iliyopelekea Mahakama
kumtafuta Wakili maarufu Mkoani Mbeya, Sambwee Shitambala kuwa Mkalimani wake
aliweza kuwatambua Watuhumiwa wote watano.
Shahidi huyo aliiambia Mahakama
hiyo kuwa Mnamo Januari Mosi Mwaka huu aliwasili Jijini Dar Es Salaam akitokea
kwao Nchini India akitumia usafiri wa ndege wa Shirika la Oman akiwa na lengo
la kufuatilia mradi wa Uchimbaji dhahabu katika Migodi ya Chunya Mkoani Mbeya
inayoendeshwa na kampuni yao ya Otro Mining.
Alisema Januari 3,Mwaka huu
alisafiri kutoka Dar Es Salaam kuja Mbeya akitumia Shirika la Ndege la
Precision ambapo aliwasili majira ya Saa Saba na Nusu Mchana na kupokelewa na
rafiki yake Isaya Mkindi ambaye walielekea naye moja kwa moja hadi Mbeya Hotel
alikopata chakula cha Mchana.
Alisema baada ya hapo alipewa
Dereva aliyemtaja kwa jina la Ezekia ambaye alimpeleka Mwanjelwa kununua
Mablanketi mawili kisha kurudi katika Ofisi ya Rafiki yake huyo ambapo
ilipofika majira ya Saa 10:45 jioni walianza safari ya kuelekea Chunya akiwa na
rafiki yake pamoja na dereva Ezekia.
Alisema wakiwa njiani
walipofika katika Milima ya Kawetere kilomita 20 kutoka Mbeya Mjini walikuta
magari mawili yakiwa yameachana kwa mita 200 ambapo walilipita gari moja na
ndipo walipokaribia gari lingine wakakutana na vijana Wanne ambao mmojawapo
aliwasimamisha na kuomba msaada wa Spana ya kufungulia tairi ya gari yao
wakidai kuwa inapancha.
Baada ya kueleza hivyo Wakili
wa Serikali aliiomba Mahakama imruhusu Shahidi huyo kama anaweza kuwatambua
Watuhumiwa jambo ambalo alitekeleza kwa kuwagusa Mshtakiwa namba moja, Tatu,
Nne na Tano kisha kuendelea na kutoa maelezo kuhusu kilichoendelea baada ya
kuombwa spana.
Shahidi huyo aliendelea kusema
kuwa baada ya Dereva wake kuwajibu kuwa hawana spana ndipo Mtuhumiwa namba tatu
ambaye ni Askari Magereza alipotoka na kurudi akiwa na pingu mkononi na
kumfunga Dereva kisha kumshusha kwenye gari na kuelekea naye kwenye gari yao
ndogo.
Aliongeza kuwa baada ya kufanya
hivyo walimshika yeye huku wakimuoneshea panga na kumwamuru asiongee neno
lolote kisha kuhamisha mizigo kwenye gari na kupeleka kwenye gari yao ambayo li
Kompyuta za Mkononi mbili, begi, mablanketi na Simu za Mkononi ambazo kabla
hawajachukua alikuwa ameshawasiliana na Mwenzie aliyoko Chunya aliyemtaja kwa
jina la Jamir Amar.
Alisema akiwa ameshikwa na
kuongeleshwa na watu hao simu yake ilikuwa ikisikika na wenzie ambao waliweza
kutoa taarifa katika Jeshi la Polisi ambalo lilifanikiwa kuwakamata muda mfupi
baada ya watu hao kutokomea na vitu vyao na baada ya wao kuachwa akiwemo Dereva
aliyekuwa amefungwa pingu kuachiwa.
Hata hivyo Wakili wa utetezi
katika kesi hiyo Ladislaus Lwekaza alimuuliza Shahidi huyo kama kweli aliwaona
watuhumiwa wakiwa eneo la tukio na siyo kalishwa maneno alijibu anawafahamu kwa
sababu aliwaona wakifanya tukio kwa sababu ilikuwa jioni kabla jua halijazima.
Wakili Lwekaza aliongeza kuwa
akiruhusiwa kuwabadilisha watuhumiwa mkao wao anaweza kuwatambua Shahidi huyo
alijibu anaweza hivyo akatakiwa kutoka nje ili waweze kuwachanganya ndipo
awatambue jambo ambalo lilipingwa na Wakili wa Serikali kuwa haijawahi kutokea
utambuzi ukafanywa wakati kesi inaendelea kusikilizwa na kuongeza kuwa jambo
hilo hufanyika kipindi cha upelelezi.
Kutokana na hoja hizo Hakimu
Mteite alikubaliana na hoja ya upande wa Mashtaka hivyo kutupilia mbali maombi
ya upande wa mashtaka ya kumtaka Shahidi atoke nje ili wamchanganyie watuhumiwa
kwa ajili ya kuwatambua na kuamuru
kuendelea na maswali mengine.
Watuhumiwa hao ni pamoja na Mshitakiwa namba moja ambaye ni Askari Polisi PC
James mwenye namba F8302 wa Wilaya ya Mbeya ambaye kabla ya kufikishwa
mahakamani alivuliwa Uaskari baada ya kuhukumiwa kijeshi.
Wengine kuwa ni
mshtakiwa namba mbili kuwa ni Elinanzi Mshana(22)Mkazi wa Iyela Jijini Mbeya,
Askari Magereza mwenye namba B 500 Sajenti Juma Mussa(37) wa Gereza la Ruanda
Mbeya,Mbaruku Hamis(29) Mkazi wa Iyela na Amri Kihenya(38) Mkazi wa Iyela.
Akisoma
mashtaka yao Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite, Basilius
Namkambe alisema watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Januari 3, Mwaka huu majira
ya saa 11 jioni katika eneo la Mlima Kawetere barabara ya Mbeya Chunya.
Alisema
watuhumiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kulizuia gari aina ya Pick Up
lililokuwa likiendeshwa na Ezekia Matatira (34) Mkazi wa Iyunga Jijini Mbeya
ambaye alikuwa na mtu aliyekuwa akifahamika kwa jina la Sreedhar Pasupelet(38)
mwenye asili ya Kiasia wakitumia magari madogo mawili ambayo ni GX 100 Toyota Cresta
T 782 BEU na Gari linguine ambalo lilikuwa na namba za Chesesi GX 6011832 aina
ya Grand Mark II.
Hata hivyo Kesi
hiyo iliahirishwa hadi Februari 13, Mwaka huu itakapoendelea tena kwa upande wa
mashtaka kuwaleta mashahidi wake.
(Habari na Ezekiel Kamanga.)
(Habari na Ezekiel Kamanga.)
Post a Comment
Post a Comment