Kufuatia kuwepo kwa vitendo vya kujichukulia sheria mkononi kunakosababishwa na imani za kishirikina, Jeshi la Polisi Nchini limeweka mkakati maalumu wa kukabiliana na vitendo hivyo.
Akiongea na Waandishi wa habari katika mahojiano maalumu, Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Advera Senso amesema vitendo hivyo ni uhalifu kama ulivyo uhalifu mwingine hivyo kuitaka jamii kutoa taarifa za wahalifu hao ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Alisema kuwa wapo wananchi wachache ambao wamejijengea mazoea ya kujichukulia sheria mkononi pindi yanapotokea matukio ya kihalifu bila kujali kuwa vipo vyombo vinavyohusika katika kushughulikia matukio ya aina hiyo likiwemo Jeshi la Polisi.
Alisema Jeshi la Polisi litaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaojichukulia sheria mkononi lakini pia watendelea kuielimisha jamii juu ya madhara ya vitendo hivyo.
Aidha Senso alisema mkakati wa Polisi uliopo hivi sasa ni kwa watendaji wake kuacha kukaa ofisini na badala yake watoke na kwenda kushirikiana na jamii katika kutatua kero za uhalifu katika jamii kama walivyoelekezwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu.
Alisema lengo kubwa la mkakati huo ni Makamanda wa Polisi kuwahamasisha na kuwahimiza wananchi ili waweze kuwapatia taarifa ambazo kwa kiasi kikubwa zitasaidia kuwabaini wahalifu pamoja na viashiria vya uhalifu na kuweza kuuzuia kabla haujatokea.
Senso ametoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika mapambano dhidi ya uhalifu na wahalifu hapa nchini ili kuendelea kudumisha usalama kwa nchi yetu.
Post a Comment
Post a Comment