GuidePedia

0


Hili ndilo jengo la zahanati ambalo bado halijaisha ujenzi wake.
Hawa ni baadhi ya wananchi wakiwa katika mkutano wa kijiji uaohusu ujenzi wa zahanati hiyo.
Hawa ni baadhi ya viongozi wa kijiji hicho wakiwa katika mkutano huo.
......................................................................................................................................................


Afisa kilimo wa kijiji cha Itamboleo kata ya Itamboleo  wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya Hebron Mwilwa anatuhumiwa kutafuna  zaidi yashilingi milioni tatu zilizotolewa na Halmashauri ya wilaya ya Mbarali kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa kijiji hicho Bwana Samweli Kaganga ambaye amesema afisa huyo alitumia fursa hiyo alipokaimu nafasi ya mtendaji alipokuwa anaumwa.

Kaganga amesema kuwa Mwilwa alichukua fedha hizo kwa nyakati mbili tofauti kutoka kwa mzabuni aitwaye Medrack Mheza aliyepewa zabuni ya kusambaza vifaa vya zahanati hiyo ambapo Serikali ilitoa milioni nane ili kuendeleza ujenzi uliokuwa umefikia hatua ya mtambaa panya.
Awali afisa kilimo alichukua kwa mkandarasi shilingi 1,587,000/- akidai kijiji kimemtuma fedha hizo kwa ajili ya ununuzi wa mbao za milango na madisha ya zahanati,mara ya pili alichukua shilingi 1,819,000/- akidai kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vingine ambapo pesa hizo hakuzifikisha ofisini bali alizitumia kwa matumizi binafsi.

Baada ya kuona shughuli ya ujenzi imekwama ambapo mwenyekiti alimfuatilia mkandarasi kujua kulikoni ndipo alipomwonesha hati ya makabidhiano inayoonesha Afisa kilimo alivyokabidhiwa fedha hizo.
Hata hivyo baada ya kuona Afisa kilimo haonekani alitoa taarifa kwa Mkurugenzi ambaye ndiye mwajiri lakini hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya Afisa huyo ambaye hajaonekana kazini takribani miezi mitatu sasa huku wananchi wasijue la kufanya.

Hali hiyo imepelekea mifuko 40 ya saruji iliyonunuliwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo kuharibika kutokana na kukosekana kwa fedha za kununulia mchanga na kulipa vibarua fedha ambazo Afisa huyo wa serikali amezitafuna bila ridhaa ya kamati ya afya na mkutano wa kijiji.
Hata hivyo Diwani wa kata ya Itamboleo Lwitiko Mwangosi alikataa kulizungumzia suala hili akidai taratibu za kitumishi zinaendelea na wananchi watapewa taarifa.

Kwa upande wake mtendaji kata Athumani Sakunja amesema kuwa alimwandikia barua ya kumtaka Afisa kilimo kurejesha fedha alizochukua ambapo aliahidi kuzirejesha mwezi Desemba mwaka uliopita lakini hakutekeleza,hivyo amemtumia waraka Polisi kata ili Afisa huyo akamatwe mara moja ili arejeshe fedha hizo.

Kwa upande wake Mbunge wa Mbarali Dickson Kilufi amesema hajapata taarifa zozote kutoka kijiji cha Itamboleo kuhusiana na tatizo hilo na kuahidi kufuatilia ili kujua mwisho wake,lakini amesema hatakuwa tayari kufumbia ubadhilifu kwa watumishi wa umma kwani wanakwamisha juhudi za serikali kuleta maisha bora kwa wananchi wake.


Post a Comment

 
Top