GuidePedia

0


Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania[UWAMATA]kanda ya Mbeya wamelalamikia Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani na Mamlaka ya Usafirishaji[SUMATRA] Mkoa wa Mbeya kwa kuwanyanyasa wawapo kazini.
Tamko hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Madereva kanda Damas Mwandumbya katika ukumbi wa Miami iliopo Kata ya Ilomba Jijini Mbeya mbele ya Mgeni rasmi Mkuu wa Polisi Mkoa ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya Robert Mayala.

Waliotuhumiwa kula rushwa ni pamoja na Askari Polisi wa kikosi cha Usalama Barabarani wa Wilaya za Rungwe na Mbeya ambapo majina yao yalitajwa mbele ya kikao hicho pamoja na Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya Butusyo Mwambelo ambaye imedaiwa kuwapa malengo Askari wake ili mgao afikishiwe kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya.

Mgao mwingine wa pesa hizo umetajwa kwenda kwa Mkuu wa Usalama Barabarani nchini na kila Dereva anapokamatwa au kusimamishwa hulazimika kutoa shilingi elfu tano au zaidi katika kila kituo anachosimamishwa ndipo gari huendelea na safari.

Hali hiyo husababisha Madereva kujaza abiria ili kukidhi malengo ya waajiri na kumudu kulipa Askari wa Usalama Barabarani na kama wasipotoa hukamatwa na kutozwa faini au kupelekwa mahabusu hali inayowafanya kufanya kazi katika mazingira magumu.

Aidha Madereva hao walimtuhumu Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa Mbeya kwa kuwafukuza ofini kwake pindi wanapohitaji huduma  na kuwa na lugha chafu inayowadhalilisha madereva hivyo mara kadhaa kugoma au kutishia kugoma kutokana na kauli za kiongozi huyo.

Mbali ya shutuma hizo kwa Jeshi la Polisi SUMATRA walilalamikiwa kwa kuruhusu magari ya aina ya NOAH ambayo yameanza kusafirisha abiria bila kukidhi vigezo hali inayosababisha baadhi ya magari ya abiria aina ya HIACE kushindwa kufanya kazi kutokana na magari hayo kufanya kazi kiholela huku Jeshi la Polisi na SUMATRA wakifumbia macho.

Akijibu tuhuma hizo Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya Robert Mayala aliwapa fursa wanaotuhumiwa kujieleza mbele ya mkutano huo uliojumuisha madereva wa COASTER na HIACE ambapo Mkuu wa Usalama Barabarani alikanusha kuwafukuza madereva ofisini kwake bali alidai kuwa viongozi wanatetea wahalifu hali hiyo isipodhibitiwa itasababisha ajali ambazo zinaweza kuepukika.

Hata hivyo Butusyo aliomba radhi endapo amewafukuza ofisini kwake madereva hiyo imekuja kutokana na dharau za baadhi ya maderva ambao wamekuwa wakidharau Askari wake hata yeye amedharauliwa kwa madereva kujaza abiria licha ya kupewa onyo.

Kwa upande wake Meneja wa SUMATRA amesema kuwa amepokea malalamiko yao na kuahidi kuyafanyia kazi malalamiko yao lakini pia Madereva wafuate sheria ili kuondoa mvutano usio wa lazima kwani madereva ni sehemu ya jamii ambao wana mchango mkubwa kwa Taifa.

Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Mbeya Robert Mayala amekiri kupokea malalamiko yao na kwamba Jeshi la Polisi litakutana na Askari wanaolalamikiwa hasa wa Wilaya ya Rungwe na amemwagiza Mkuu wa usalama Barabarani kurekebishwa kasoro zote ili kila upande ufanye kazi kwa amani.

Alihitimisha kwa kuwataka Madereva kutii sheria bila shuruti ili kuepusha ajali na kuwataka madereva wakatae kutoa rushwa na Askari atakaye walazimisha watoe taarifa kwake ambapo aliwapatia namba zake za simu yake ili kupata taarifa kwa haraka.

Post a Comment

 
Top