GuidePedia

0
Huyu ndiyo mwanamke aliyejifungua watoto watatu huko wilayani chunya mkoani mbeya.
......................................................................................................................................


Mwanamke mmoja anayefahamika kwa jina la Paskalia Adrofu [37]mkazi wa kijiji cha Magamba kata ya Magamba wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya,amejifungua salama watoto watatu hivi karibuni.

Paskalia amejifungua watoto wawili jinsi ya kiume na mmoja wa kike ambapo amesaidiwa  na mkunga wa jadi aitwaye Dotea Mwanakulya [60]anayeishi kijiji cha Magamba.

Paskalia amesema kwamba mume wake aitwaye Richard Saba [55] ni mkulima hivyo imekuwa vigumu kwake kumudu gharama za matunzo kwa watoto hao ambapo ana jumla ya watoto wanane,wakiwemo mapacha ambao wamemaliza shule ya msingi na hawajachaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari.

Mama huyo alianza kujifungua mtoto wa kwanza mwaka 1995,wa pili ambao ni mapacha mwaka 1998 wa tatu mwaka 2006,wa nne mwaka 2009 na wa tano ambao wamezaliwa watatu amejifungua mwanzoni mwa mwaka huu ambao wana afya njema.

Hata hivyo Paskalia amesema uongozi wa kata akiwemo Diwani wa kata ya Magamba mheshimiwa Chakupewa Kapalala wamefika kumtembelea na kumjulia khali yake na kumhimiza kuhudhuria kliniki mara kwa mara ili kufuatilia afya za watoto.

Aidha mkazi mmoja wa kijiji hicho aitwaye Luhende Luhaga ametoa ng’ombe wawili wa maziwa ili mama huyo amudu kuwanyonyesha watoto hao bila shida kutokana na kulemewa na watoto hao.
Watoto wawili wa mwanzo wamezaliwa na uzito wa kilo 2.8 na wa tatu amezaliwa na uzito wa kilo 2.0 ambapo Paskalia amesema kuwa watapofikia uzito wa kilo 3 ndipo watapatiwa chanjo katika zahanati ya Magamba.
Baadhi ya changamoto anazokabiliwa nazo ni pamoja na nguo za watoto,chupa za kunyonyeshea,sabuni,mafuta na chupa za chai kwa ajili ya kuhifadhia maziwa ya watoto.
Kwa upande wake Mkunga wa jadi aliyemzalisha Paskalia amesema anakabiliwa na changamoto za ukosefu wa vifaa vya kujifungulia kama kitanda,godoro,mipira ya kuvaa mikononi ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa ambapo wagonjwa wengine hufika hapo wakiwa hawana vifaa  hivyo.

Hata hivyo mkunga huyo amewaomba wadau mbali mbali kumsaidia kupata daftari ya kutunza kumbukumbu za watoto wanaozaliwa.

Post a Comment

 
Top