GuidePedia

0


Mwenyekiti wa kamati ya Afya kijiji cha Malangali  Kata ya Totowe wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya Ahmed Ndauka amejiuzuru kufuatia Kamati ya Afya ya Kijiji na Wilaya kufumbia uovu unaofanywa na Muuguzi katika Zahanati ya Kijiji hicho.

Ndauka akiongea kwa masikitiko juu ya vitendo viavyofanywa na muuguzi huyo Pilly Ntongolo amesema amekuwa akiwanyanyasa wagonjwa kwa kuwatoza pesa za dawa pamoja na vifaa vya kujifungulia wajawazito ambavyo vinapaswa kutolewa bure kwa mujibu wa sera ya Afya.

Baadhi ya wananchi wametoa taarifa kwa Diwani wa Kata ya Totowe Godian Wangala ambaye amewahi kumwita na kumuonya mara kadhaa lakini amekuwa akikaidi kwa kile kinachodaiwa kuwa kuna mtu anayemlinda wilayani.

Matukio ya hivi karibuni ambayo yametukia katika Zahanati hiyo ni pamoja na kumtoza mjamzito mmoja kiasi cha shilingi elfu kumi na moja kwa mgonjwa kwa ajili ya huduma ya kujifungua kwa mama huyo ambaye alifika majira ya saa kumi na mbili jioni akiwa ameletwa na nduguze wawili.

Muuguzi alipokea malipo ya awali ya shilingi elfu sita akidai ni kwa ajili ya vifaa vya kujifungulia ambavyo hakuvitoa na yeye kwenda kwake na kuuchapa usingizi akimwacha mgonjwa na nduguze ambapo alijifungua  salama kwa kusaidiwa na ndugu zake.

Hata hivyo muuguzi huyo alipofika asubuhi badala ya kuwashukuru ndugu waliomzalisha mgonjwa aliwataka waongeze shilingi elfu tano kwa ajili ya kadi  ya kliniki na vifaa vya  kujifungulia ambavyo muuguzi huyo hakuvitoa.

Baada ya ndugu kukerwa na tabia ya muuguzi huyo waliamua kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Afya Bwana Ahmed Ndauka ambaye aliitisha baadhi ya wajumbe na kwenda Zahanati kuonana na muuguzi lakini walipofika uuguzi alimrukia Ndauka na kumchania shati hali iliyowashangaza wajumbe.

Baada ya tukio hilo Ndauka alitoa taarifa kwa Mtendaji wa kijiji Yaledi Mwanguku ambaye alifika na kushuhudia tafrani hiyo na kutaka suala hilo likajadiliwe katika uongozi wa kijiji.

Aidha kabla ya suala hilo kujadiliwa kijijini Muuguzi huyo aliandika barua wilayani akidai kuwa amepigwa na Ndauka kitu ambacho si kweli ambayo ilimshangaza na kamati ya afya ilifika kijijini hapo na kumkandamiza Ndauka akubaliane nao hali ambayo haikumpendeza na kuamua kuandika barua ya kujiuzuru.

Muuguzi huyo amekuwa akilalamikiwa na wananchi wa kijiji hicho kwa kuwatoza dawa ambazo nyingine zinapaswa kutolewa bure.
Pamoja na kujiuzuru wadhifa huo Ndauka amesema atabainisha ukweli kwa wananchi waliomchagua kwani ndio wenye dhamana ya kubaini ukweli dhidi ya tuhuma za muuguzi huyo.

Kwa upande wake Pilly Ntongolo amesema yeye alimuuzia mpira mgonjwa wake usiku huo kwani muda wa usiku maduka hufungwa na kama muuguzi alimsaidia ili mtoto azaliwe salama,pia alikanusha kuuza dawa bali kila dawa hutolewa kwa utaratibu maalumu.

Aidha aliwataka wananchi wanaokuja kupata huduma  ya uzazi waje na vifaa wanavyoelekezwa ili kuondoa marumbano ambayo hayana tija na kumvunja moyo wakati yeye hapo kazini hana msaidizi yeyote hivyo kufanya kazi kuwa ngumu kwake.


                                                                           (Na, Mwandishi wetu)

Post a Comment

 
Top