GuidePedia

0


Mtendaji wa kijiji cha totowe Caristo Mwamandaaliyejishika kichwani.
wananchi wa kijiji cha totowe wakiwa katika mkutano wa kijiji hicho




Wananchi wa kijiji cha Totowe Kata ya Totowe wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya wameulaumu uongozi wa kijiji kwa kutofanya mikutano ya kijiji kwa mwaka mzima hivyo kuamua kuivunja serikali yote ya kijiji kutokana na kuzorotesha maendeleo ya kijiji kutokana na ubadhilifu wa zaidi ya shilingi milioni thelathini na sita.

Hayo yamebainishwa na wananchi hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo ambao ulihudhuriwa na mtendaji Kata Ronward Mwashiuya ambapo Mwenyekiti wa Kijiji Gido Namwene na serikali yake wanashutumiwa kwa kutofanya vikao na hivyo kusababisha ufujaji wa fedha za kijiji.

Baadhi ya miradi inayolalamikiwa ni pamoja na uuzwaji wa tofali 26000 za ujenzi wa  nyumba za walimu shule ya msingi Totowe tofali ambazo zimetoweka katika mazingira ya kutatanisha hivyo kudhoofisha juhudi za wananchi.

Mbali ya tuhuma hiyo pia Mtendaji wa kijiji hicho Caristo Mwamanda ambaye ameondolewa kutokana na ubadhilifu wa shilingi laki moja ambapo Mwenyekiti Gido baada ya kubanwa alikabidhi jumla ya shilingi laki moja ambazo mtendaji alizitafuna bila ridhaa ya wananchi.
Hata hivyo baada ya tuhuma hizo Mtendaji Mwamanda alitimuliwa kijijini hapo na kuhamishiwa kijiji cha Ifuko na kuletwa Mtendaji mwingine Adamson Mwaitege ambaye ameanza utaratibu wa kusoma mapato na matumizi mwaka huu.

Aidha wananchi wamelalamikia kamati mbalimbali za kijiji hicho ikiwemo kamati ya huduma za jamii ambapo kamati hiyo inatuhumiwa kuuza viwanja kiholela na baadhi ya viwanja kumilikiwa na viongozi wa kamati ya huduma ya jamii.

Mtendaji Kata ameonya utaratibu wa ugawaji viwanja haukufuatwa na isipozingatiwa kutatokea mgogoro mkubwa wa ardhi na kutotolewa stakakabadhi za serikali na amezitaka kila kamati kuwa na kitabu cha kukusanyia mapato ili kutunza kumbukumbu sahihi za fedha za serikali.
Mkutano huo ulishindwa kuafikiana na kamati zote ikiwa ni pamoja na makusanyo ya fedha za adhabu mbalimbali kama kuzagaa kwa mifugo ambapo fedha za tozo zimekuwa zikiishia mikononi mwa wachache na waliotozwa wamekuwa hawapewi stakabadhi na kufanya kijiji kukosa mapato.

Waliotimuliwa ni pamoja na Mwenyekiti Gido Namwene,Mtunza hazina Benard Kihinda na wajumbe Charles Jampani,Erasto Darweshi,Oliva Kasekwa,Michael Patrick,Simon Erick na Doctor Yalinga.
Wengine ni pamoja na Charles Mnyuzi,Juma Lwamba,Jacob Lupila,Bosco Mnyuzi,Maria Soda na George Mnyuzi.

Katika serikali hiyo imebakiwa na Mtendaji wa Kijiji Adamson Mwaitege ambaye wakati wa matukio hayo yeye alikuwa hajahamia kijijini hapo hivyo hakuguswa na tuhuma hizo mkutano uliridhia yeye ndiye afanye shughuli za Mwenyekiti katika kipindi cha mpito.
Mtendaji Kata Ronward Mwashiuya amesema utaratibu uliotumika katika mkutano huo wa kuiondoa serikali ya kijiji umekiukwa kutokana na hesabu hizo kutokaguliwa na mamlaka husika na kama mamlaka hiyo baada ya ukaguzi kama ikibaini ndiyo yenye dhamana ya kuwafikisha watuhumiwa kwenye vyombo vya sheria.

Mkutano ulimalizika kwa amani kutokana na hekima za mtendaji Kata kuwaomba wananchi kupunguza jazba hadi hapo suala lao litakapopatiwa ufumbuzi na ngazi za juu.

                                                   Na, Ezekiel Kamanga.

                                                    Lumemo blog


Post a Comment

 
Top