GuidePedia

0


baadhi ya viongozi wa kamati hiyo pamoja na viongozi wengine wa kijiji wakiwa meza kuu katika mkutano huo.



baadhi ya wananchi wakiwa katika mkutano huo

baadhi ya wajumbe wakionesha karatasi mbali mbali zinazohusu tuhuma hizo.

Hii ni moja kati ya bili ya maji zilizolipwa na wananchi.

Hii ni hati ya kukiri ya viongozi hao wa badhirifu wa kamati hiyo, kuhusu kutumia fedha kwa manufaa yao binafsi.







Kamati ya maji ya kijiji cha Iwanga Kata ya Utengule Usongwe Wilaya ya Mbeya inatuhumiwa kwa ubadhilifu wa fedha za mradi wa maji zaidi ya shilingi milioni mbili zilizochangwa na wananchi wa kijiji hicho.

Tuhuma hiyo imebainishwa na Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na wananchi wa kijiji hicho baada ya kuitishwa mkutano wa hadhara hivi karibuni.

Wanaotuhumiwa kwa ubadhilifu huo ni pamoja na Semu Jaton,Enitha Mathayo,Daud Mwampashi,Langton Mwawayo na Makala Mwakalemba.

Mwenyekiti  wa Tume ya Uchunguzi Grace Jerema amesema kuwa baadhi ya viongozi wa kamati hiyo walichukua fedha benki katika akiba ya mradi wa maji kwa matumizi yao binafsi bila ridhaa ya wananchi.

Jerema amesema Tume yake imebaini mnamo Septemba 19,mwaka 2012 Semu Jaton kwa kushirikiana na Anitha Marijani walichota shilingi elfu sitini kutoka Benki ya NMB,Desemba 12 mwaka 2012 walichota shilingi laki moja ambazo pia walitumia kwa matumizi yao binafsi.

Baada ya kubanwa na wananchi walikiri kuchota pesa hizo bila ridhaa ya wananchi na kuamua kuzirejesha benki, hivyo wananchi kukosa imani na kamati kwa vile Mwenyekiti wa kamati Julius Mwendo na Mtunza Hazina Christina Mpunga hawakushirikishwa kwa kuwa wao hawana saini zao Benki.

Kamati ya uchunguzi pia ilibaini kuwa baadhi ya fedha nyingine zilizokusanywa zilichotwa na Viongozi wa Serikali ya Kijiji akiwemo Mwenyekiti Aleck Mwasubila aliyedaiwa kujichukulia shilingi laki nne na ishirini elfu,Mtendaji Kata aliyehamishwa Lwitiko Mwaibindi ,Mafundi Bomba Lington Mwalingo anayedaiwa kuchota laki moja tisini na nane elfu na Makala Mwakalemba aliyetafuna shilingi elfu hamsini na mbili ambao wote walitajwa katika Tume ya Uchunguzi.

Mbali ya tuhuma hizo Tume imebaini kuwa kuna vitabu vilivyokuwa vinatumiwa na Uongozi wa Kijiji bila kushirikisha Kamati ya maji hali inayotia shaka kama fedha za maji zilitumika kama ilivyoazimiwa katika vikao.

Tume ilipokamilisha uchunguzi wake ilikabidhi nakala ya taarifa ya uchunguzi kwa uongozi wa kijiji na kuomba kuitishwa mkutano Mkuu wa kijiji ili taarifa hiyo isomwe mbele ya wananchi lakini kulitokea marumbano baina ya Tume na Serikali kwani Serikali ikitaka kupatiwa nakala halisi.

Aidha Kamati ya Uchunguzi ilisita kukabidhi nakala halisi Serikalini kwa kuhofu kuhujumiwa hivyo kuomba ipelekwe ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ili ukaguzi ufanyike na watakaobainika wachukuliwe hatua za kisheria.

Kutokana na marumbano hayo vikao viwili viliitishwa bila mafanikio kijijini hapo na kulazimu uongozi wa Kata kuamua kuitisha kikao kingine Februari 26 mwaka huu kupitia kwa Afisa Maendeleo ya Jamii Kata Martin Gowele ambaye pia ni Kaimu Afisa Mtendaji Kata ili kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Katika mkutano uliofanyika kijijini hapo Gowele aliagiza kuwa Kamati ya Uchunguzi ivunjwe na kukabidhi nyaraka zote vikiwemo vitabu vya kukusanyia fedha ili kazi ya makusanyo iendelee kama awali kupitia mradi wa maji.

                            


                                  Na, Ezekiel Kamanga

                                         Lumemo blog



Post a Comment

 
Top