GuidePedia

0

SERIKALI wilayani Rungwe mkoani Mbeya jana ilisalimu amri kwa wenyeviti wa serikali za vijiji baada ya wenyeviti hao kutangaza mgomo wa muda usiojurikana kufanya kazi za serikali katika vijiji vyao wakiishinikiza serikali kupitia halmashauri hiyo kuwapa stahiki zao.


Hatua hiyo ilifanyika baada ya mkuu wa wilaya ya Rungwe Chrispin Meela akiwashirikisha  mwenyekiti w a halmashauri  Mwakipiki Mwakasangula pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kuitisha mkutano na wenyeviti wote wa jimbo la Rungwe magharibi katika ukumbi wa CCM kwa lengo la kuwataka waendelee kufanya kazi wakati suala lao linashughurikiwa.


Katika mkutano huo uliokuwa na hisia tofauti huku mkuu wa wilaya akiwatoa nje ya ukumbi waandishi wa habari kwa madai kuwa mkutano huo uliwahusu wajumbe pekee  ambapo aliwataka wenyeviti kuwa na subira kwa kuwa suala la posho mbali na kuwa bunge lilitangaza lakini bado utekelezaji haujaanza na kuwa wanatakiwa wafanye mikutano kwenye kamati za maendeleo ya kata (KAMAKA) na mihutasari waipeleke katika ofisi yake ili ianze kufanyiwa kazi  kwenye vikao vyake vya DCC.


“Ni kweli mnafanya kazi katika mazingira magumu ninawaomba tengueni mgomo,fanyeni kazi huku mkiendelea kufanya mikutano katika vijiji vyenu,mimi ninaenda Dodoma kikazi nitakaporejea tutafanya mkutano kama huu tena ili kupeana mrejesho wa wapi mlipofikia huku suala la semina mwenyekiti wa halmashauri anaendelea kulifanyia kazi” alisema Meela.


Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mwakipiki  Mwakasangula kwa upande wake mbali na kuwapongeza wenyeviti hao kukubali kufanya kazi alisema kuwa hakutegemea kuwa mkutano huo utafanyika kwa amani kutokana na jazba walizokuwa nazo wenyeviti hao na kuwa atahakikisha kuwa wataanza kupata semina siku za usoni huku wakitafuta namna ya kuweza kuwapa posho.


Katibu wa wenyeviti  hao jimbo la Rungwe Magharibi Jonhs Mwakalendile alisema kuwa anapongeza hatua ya serikali wilayani humo kusikia kilio chao cha kutowapa posho na kuwa maagizo waliyoyatoa wayatekeleze ili waweze kuendelea kufanya kazi kama zamani na kuwa wametumika sana katika shughuri za maendeleo bila posho wala semina hivyo kama suala hilo litafanyiwa kazi hawana budi kuendelea na kazi huku wakivuta subira ya kupewa stahiki zao.


Alisema kuwa Serikali imeshindwa kutambua jitihada zao na ndiyo maana imekuwa haiwathamini wakati serikali inaanzia kwenye vijiji lakini wao wanatoa posho kwa madiwani na maafisa watendaji na wabunge na kuwa katika bunge la katiba linalotarajiwa kuanza siku za usoni serikali imepanga posho Tsh,300.000 kwa siku huku wao wakiendelea kupata shida na familia zao na kugeuzwa misukule au mazombi kwa kuzidi kutumikishwa.


“sisi tumekuwa chachu ya maendeleo katika serikali kwa kuchangisha michango na kusimamia ujenzi wa miradi ya maendeleo lakini serikali imeshindwa kuthamini jitihada hizo kwa kuwa DC ameahidi kumaliza tatizo hili katika siku za usoni basi tutaendelea kufanya kazi kwa moyo mmoja huku jicho letu likiwa kwake kama mambo yatakuwa ni yaleyale basi wataedesha mgomo wa majimbo yote mawili pamoja na kufanya maandamano makubwa”alisema Mwakalendile.


Wenyeviti hao wa jimbo la Rungwe Magharibi walifanya mgomo huo wiki iliyopita wakiishinikiza serikali iwape stahiki zao baada ya kusikia kauli ya Bunge lililoketi Augost 31 mwaka jana kuwa posho za wenyeviti zinapelekwa kwenye halmashauri za wilaya kila mwaka na wao wakaamua kudai posho hizo kwa madai kuwa posho zao zinaliwa na wakubwa huku wao wakiendelea kupata taabu.

 

                                                    

                                             Na Ibrahim Yassin,
                                               
                                              Lumemo blog

Post a Comment

 
Top