GuidePedia

0



KANISA la Moroviani Jimbo la Kusini Magharibi lenye makao makuu Mkoani Mbeya limeingia katika mgawanyiko mkubwa baada ya viongozi, Wachungaji na Waumini kutoelewa kutokana na kuvuliwa uongozi kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jimbo hilo.

Mwenyekiti aliyesimamishwa uongozi ni Mchungaji Nosigwe Buya ambapo baadhi ya Watumishi, Waumini na Wachungaji wa Kanisa hilo kupinga maamuzi ya kuondolewa kwa Mwenyekiti kwa madai kuwa maamuzi hayo yalikiuka katiba ya katika.

Kutokana na kuwepo kwa mtafaruku ndani ya kanisa hilo, Baadhi ya Wachungaji wapatao 25 wa kanisa hilo walijitokeza mbele ya vyombo vya habari wakitoa tamko kali la kuutaka kurejeshewa kwa madaraka yake Mwenyekiti huyo ili kunusuru kuvunjika kwa kanisa.

Wachungaji hao ambao walimchagua Mchungaji Chilale Edward Simoni kuwa Mwenyekiti wao na Daudi Mwiligumo kusoma tamko waliloliandaa linalopinga maamuzi ya kusimamishwa uongozi Mwenyekiti wao wa Jimbo na kuitaka Mahakama kuingilia kati.

Akisoma tamko hilo, Mchungaji Mwiligumo alisema jambo wanalopingana nalo ni  pamoja na kikao cha kumsimamisha Mwenyekiti kilivunja katiba ya kanisa iliyosahihishwa na kusanifiwa mwaka 2012 ibara ya 11 kifungu cha 4(iv).

Alisema kifungu hicho kinasema Mwenyekiti asipokuwepo, Makamu mwenyekiti atakuwa mbadala yake na ibara ya 35 inasema wakati wowote Mwenyekiti asipokuwepo Makamu atakuwa Mwenyekiti lakini katika kikao kilichomuondoa Mwenyekiti wao hata Makamu hakuwepo hivyo kikao kilikosa uongozi.

Aliongeza kuwa katika kikao kilichofanyika Julai 31, Mwaka jana kilimuondoa Katibu Mkuu ambaye kwa mujibu wa Katiba ibara ya 36(2)(ii) ambacho kinataja moja ya kazi za katibu ni kuandika Muhtasari wa kikao  hivyo kikao hicho hakikua halali kutokana na watendaji wakuu kutokuwepo.

Tamko hilo liliendelea kudai katiba ya kanisa hilo iliendelea kuvunjwa baada ya Muumini wa kawaida aliyetajwa kwa jina la Charles Mwakipesile kukalia kiti kinyume cha ibara ya 10(2)C ambacho kinasema Mwenyekiti na makamu sharti wawe wachungaji.

Walisema kwa mujibu wa katiba mwenyejukumu la kumuondoa kiongozi yeyote katika nafasi yake ni Mkutano mkuu wa Sinodi unaohusisha wajumbe wengi na kwamba Mwenyekiti aliyeondolewa alichaguliwa kihalali na Sinodi mwaka 2012.

Mbali na hilo wachungaji hao walidai vipengere vingine kukiukwa ni pamoja na kumdalisha kazi Mwenyekiti huyo kinyume na utaratibu ikiwa ni pamoja na kumpangia katika kituo kipya cha kazi ambayo ni ya chini kuliko wadhifa aliyokuwa nao.

Pia walipinga kitendo cha Kutakiwa Mwenyekiti huyo kuhama katika nyumba za kanisa hadi kufikia Februari 7, Mwaka huu kinyume cha utaratibu uliwekwa na kanisa hiloambao kila kiongozi wa Kamati tendaji hutakiwa kuishi katika nyumba zilizo ndani ya Makao makuu ya Jimbo.

Waliongeza kuwa juhudi zao zote ni kutaka kulinusuru kanisa na kuiomba Mahakama na vyombo vya Dola kuingilia kati kwa kumtambua Mwenyekiti wa Jimbo Mchungaji Buya kuwa ndiye Mwenyekiti halali wa Jimbo na kuiamuru Halmashauri ya jimbo na kamati tendaji pamoja na Askofu Alinikisa Cheyo kuitisha Mkutano wa Sinodi haraka kwa ajili ya maamuzi.

Aidha mgogoro unaoendelea ndani ya kanisa hilo pia umemhusisha moja kwa moja Askofu wa jimbo hilo, Alinikisa Cheya na kwamba kuna watu wachache wanataka kulitumia kanisa kama taasisi binafsi kujinufaisha wao wenyewe.


                                                                               (Na, Ezekiel Kamanga)

Post a Comment

 
Top