GuidePedia

0
IMEELEZWA kuwa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya kishirikina kwenye kitongoji cha Seko Kijiji cha Njisi kata ya Katumbasongwe Wilayani Kyela mkoani Mbeya wananchi wa kitongoji hicho wameuomba uongozi wa Serikali ya Kijiji kuwapa kibali cha kumwita Mganga wa jadi (SANGOMA) kuja kuwasaka wanaofanya vitendo hivyo vya kishirikina nyakati za usiku.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana kijijini humo kwa nyakati tofauti wananchi hao walidai kuwa kitongoji chao kimeingia doa baada ya kufanyiwa vitendo vya kishirikina nyakati za usiku kama kufanya tendo la ndoa,upotevu wa pesa kitatanishi,vishindo kusikika juu ya bati usiku wa manane na milango kugongwa na pindi wanapotoka nje hawaoni kitu.

Walisema kuwa mbali na kufanyiwa vitendo hivyo pia wamekuwa wakifanyishwa kazi mashambani nyakati za usiku bila ya wao kujua na wanapo amka hasubuhi hujikuta wamechoka mwili mzima hali ya kuwa walilala katika nyumba zao.

Kufuatia vitendo hivyo wananchi hao waliamua kuitisha mkutano wa hadhara na kuwaomba viongozi wa kitongoji na kijiji wawape ridhaa ya kwenda kumwita mganga wa jadi(SANGOMA) nchi jirani ya Malawi ili alipatie ufumbizi suala hilo.

Walisema uongozi wa kijiji walisikia kilio chao na kuamua kuwapa ruhusa ya kumwita mganga huyo na kufanya zoezi hilo kwa amani bila kuvunja amani na utulivu uliopo ambapo siku iliyofuata mganga huyo alifika na kuanza kazi ya kukagua nyumba hadi nyumba na kuwabaini watu saba ambao nao walikiri na kuomba msamaha.

Akizungumzia suala hilo mwenyekiti wa Kitongoji cha Seko Gorden Mwaikeneke aliliambia gazeti hili kuwa wananchi waliamua kufanya hivyo baada ya kutendewa vitendo hivyo kwa muda mrefu na mganga alipofika aliwabaini watu saba ambao walitolewa vipembe,hirizi,shanga na vibuyu vilivyokuwa na vitambaa vyeusi vilivyozungushiwa shanga.

Alisema watu hao waliobainika walitozwa faini ya laki 3 kila mmoja lakini katika utetezi wao mganga aliwapunguzia ambapo watu wawili walitao Tsh,200,000 kila mmoja na watu wanne walitoa Tsh,100,000 kila mmoja na mmoja alitoroka huku idadi iliyokusanywa ilifikia Tsh,800.000 ambazo aliondoka nazo mganga kama ujira wake kutokana na kazi aliyoifanya.

Alisema kuwa kufuatia hali hiyo wananchi walikubaliana kuwa iwapo watu hao wataendelea kufanya vitendo hivyo basi watafungasha virago na kukihama kitongoji hicho kwani hawatakuwa tayari kuishi na watu kama hao wanaofanya vitend vya kishetani.

Afisa mtendaji wa Kijiji cha Njisi Filimoni Mwafyungulu kwa upande wake alisema kuwa wananchi walifanya hivyo kama walivyokubaliana wao kama viongozi hawakuhusika kwa kuwa Serikali ya Tanzania haiamini uchawi hivyo walichokifanya wao ni kusimamia na kuhakikisha uvunjifu wa amani usitokee na ndivyo hali ilivyo kuwa zoezi lilifanyika kwa utulivu.

                                                     Na, Ibrahim Yassin
   
                                                     Lumemo blog

Post a Comment

 
Top