JUMUIA ya wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani
Nkasi mkoani Rukwa imetoa msaada wa magodoro 50 kwa Wanafunzi wa kike wanaoishi
hostel katika shule ya sekondari Mkwamba na kuondokana na adha ya kulala
chinimi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo katibu wa
jumuia ya wazazi CCM wilayani Nkasi Bashiru Kambarage amedai kuwa
jumuia hiyo imelazimika kutoa msaada huo baada ya kujionea changamoto ya watoto
hao wa kike walipoitembelea shule hiyo wakati wa sherehe za jumuia hiyo ya wazazi
ambazo kimkoa zilifanyika kata hiyo ya Mkwamba ambapo waliweza kujionea
mazingira magumu wanayoishi watoto hao kwa kulalia misengele na mifuko ambayo
imefunikwa kanga.
Alisema kufuatia hari hiyo CCM iliahidi
kuwapatia wanafunzi hao wanaoishi hostel magodoro 25 na kuwa baada ya
kurudi ofisini waliona kuwa idadi hiyo ya magodoro ni ndogo na kuamua kutoa
magodoro 50 ambayo sasa ameyakabidhi ikiwa ni pamoja na Tshs,155,000 ambazo
zitatumika kununulia pazia za kwenye mabweni ya wanafunzi hao ikiwa ni pamoja
na vioo kwa ajiri ya madirisha ambayo yamepasuka.
Katibu huyo wa jumuia ya wazazi alidai kuwa mazingira
wanayosomea wanafunzi katika shule hiyo ni magumu hususani kwa watoto wa
kike na kuwa ili kuweza kukabiliana na mimba mashuleni kulingana na mazingira
yenyewe ni azima watoto hao wa kike waishi hostel ambako nako watajengewa
mazingira rafiki na kupata fursa nzuri ya kujisomea na kuweza kufanya vizuri
kwenye mitihani yao.
Akipokea msaada huo kaimu afisa elimu sekondari wa
wilaya Nkasi Fortunatus Kaguo aliishukuru jumuia hiyo ya wazazi kwa msaada huo
na kuwa ili mtoto aweze kufanya vizuri na kuwa na maendeleo mazuri ya elimu
inahitaji aishi katika mazingira mazuri na kuwa CCM wamelitambua hilo na wao
kwa upande wao watauenzi msaada huo kwa kuhaskikisha kuwa vifaa hivyo vinadumu
kwa muda mrefu.
Alisema kuwa kazi iliyofanywa na CCM ilibidi ifanywe
na serikali na kuwa kwa vile serikali ina mambo mengi ya kufanya inahitaji pia
misaada kutoka kwa wadau wengine kuchangia shughuli kama hizo za maendeleo na
kuwa jumuia hiyo imeonyesha mfano na kutaka watu wengine na taasisi mbalimbali
kujitoa ili kusukuma haraka maendeleo ya elimu hapa nchini.
Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo
Morris Buberwa alionyesha kufurahishwa na misaada hiyo na kuwa
itawapunguzia kero wanafunzi hao ya kulala chini na kuwafanya wawe na afya
itakayowafanya wazingatie masomo yao na kuweza kufanya vizuri.
Awali katika taarifa yao ya shule ya sekondari Mkwamba
iliyosoma na makamo mkuu wa shule hiyo Lukuta Andrew ilisema kuwa shule
hiyo ina changamoto nyingi na kubwa ni la watoto kukatishwa masomo yao kwa
sababu ya kupata ujauzito na kuwa kwa mwaka huu tu wanafunzi wawili wa kidato
cha tatu wamepata mimba na taarifa amepelekewa afisa mtendaji wa kata
lakini wamekuwa hawapati mrejesho wa taarifa juu ya mwenendo wa kesi hizo.
Na, Lumemo blog.
Post a Comment
Post a Comment