GuidePedia

0

          mwenyekiti wa Ipc Frank Leonard akizungumza na  wahabari  hivi karibuni ,kushoto ni katibu mtendaji wa IPC Francis Godwin
.........................................................................................
Ndugu  wanahabari awali ya  yote  tunapenda  kuwapongeza  kwa  kuitikia  wito    huu wa ghafla zaidi.

Lengo la  kukutana  hapa asubuhi ya leo ni  kutaka  kujitathimini mwenendo  wa  utendaji kazi  wetu na  wadau  wanaotuzunguka ikiwemo jamii nzima .

Ndugu  wanahabari  kwa  muda sasa wanahabari  mkoa  wa  Iringa  tumekuwa na mahusiano mazuri na wadau  wetu  na jamii  nzima  inayotuzunguka kwa  kuendelea  kufanya kazi kwa  ushirikiano mkubwa jambo ambalo ni  la  kujipongeza .

Leo mbali ya  kuitana kwa ajili ya  kujitathimini mwenendo  wetu bado  tuna haja ya kuendelea kuikumbusha  jamii na  wadau  wote  kuwa chombo  cha habari na mwanahabari  si mali  ya mtu mmoja kwani mwanahabari  yupo kwa ajili  jamii nzima

Ninasema  hivyo    kutokana na kauli na matukio  mbali mbali yanayoanza  kujitokeza hasa  kutoka kwa  wana siasa  wa  vyama  vya siasa  dhidi ya wanahabari mkoani kwetu.

Wapo baadhi ya wana siasa ambao  wameendelea  kujenga  chuki binafsi  dhidi ya chombo fulani ama mwanahabari fulani kutokana na  sababu  wanazozijua  wao  jambo ambalo si jema kuendelea kulifumbia macho .

Chuki  hizi ambazo  zilikuwa  zikifanyika chini chini bado   zilikuwa zikiwafikia  wanahabari hao  kutoka kwa vyanzo  vyao  ama mwanahabari mwingine ambae labda mwanasiasa ama chama cha siasa kimekuwa kikimwona anafaa.

Ifahamike  kuwa wana siasa huona bora mwanahabari ama  chombo  cha  habari pale ambapo  wanahitaji  kukutumia na baada ya  kumaliza kufanya  hivyo  wanasiasa hao hawakuoni  bora  tena ,hivyo napenda ifahamike  kuwa wanahabari tunapofanya kazi na  wana siasa  ni lazima kulitambua  hilo huku tukijivunia taaluma  yetu  na ni vema kwa  kila kazi  tunayoifanya ni lazima  kuzingatia maadili ya tasnia hii ya habari .

Mwaka 2010 wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM baadhi ya  wanahabari  walinyanyasika zaidi katika  mkutano wa CCM na miongoni mwa  waliopatwa na misuko suko hiyo ni pamoja na mwandishi wa Habari  leo Frank Leonard ambae aliondolewa katika mkutano na vijana  wa ulinzi wa CCM.

Pia mwandishi wa  gazeti  la Tanzania daima mkoani hapa Gustav Chahe  pia  alikutwa na tukio  kama  hilo akiwa katika mkutano wa  serikali ya mtaa huko Kihesa  alifukuzwa na hata kunusurika kipigo na viongozi wa eneo hilo ambao walikuwa  hawapendi mambo  yao kufikishwa katika  vyombo  vya habari.

Pia  wapo  wanahabari ambao  wamevunjiwa  kamera  zao ama kupigwa pindi  wanapotimiza  wajibu  wao.

Mbali ya  matukio  haya kutulia na  wanahabari  kuendelea  kutimiza majukumu yao  bila ya kuingiliwa tukio kama  hilo limeweza  kujitokeza tena katika mkutano wa chama  cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) mkutano uliokuwa ukifanyika katika  uwanja wa Mwembetoka tarehe 4/6/2014 mgeni rasmi mwenyekiti wa  kamati ya hamasa kanda  John Mwambigija alitumia mkutano  huo kuvishambulia vyombo vya habari na hata  kuhamasisha wananchi kuchukia chombo kimoja wapo  cha utangazaji mkoani Iringa jambo ambalo si sahihi.

Kwani  kitendo cha  kiongozi huyo kufanya  hivyo ni  kupandikiza  chuki kati ya  watenda kazi wa  chombo  hicho ,chombo chenyewe na wadau wanaotegemea kupata habari kupitia chombo  hicho na  wanahabari hao.

Hivyo kama  chama  cha wanahabari  mkoa  wa Iringa ambao tunapenda  kuona suala la uhuru wa  vyombo  vya habari linaendelea kukua na si kufinywangwa na mtu ama  watu fulani  hatujapendezwa na kauli  kama  hizo za kichochezi  ambazo zinafifisha uhuru wa  vyombo  vya habari na kupandikiza  chuki zimekoma mara moja kwa  vyama vyote vya siasa na wanasiasa.

Rai yetu kwa  vyama  vyote  vya siasa na wana siasa ni vema  watambue  kuwa chombo  cha habari ama  mwanahabari si tawi la chama chochote  wala mali ya mwanasiasa ,japo  vipo  vyombo  ambavyo ni mali ya chama fulani  mfano  gazeti la Uhuru na Mzalendo ,hivyo  basi tunapenda kuwakumbusha  kuwa ni vema vyama na wanasiasa  kutimiza  wajibu  wao bila ya kugombanisha wanahabari na  vyombo  vyao na tusingependa  kuona uchochezi kama  huo unaendelea  kwani iwapo  uchochezi kama  huo utafumbiwa macho leo yawezekana kwa chombo  hicho  kesho  ikawa kwa  chombo kingine na ama mwanahabari mwingine .

Mwisho ningependa  kuwakumbusha   wanahabari  wenzangu  kuendelea kutimiza  wajibu  wetu kwa uhuru  zaidi bila kukiuka maadili ya tasnia  hii pili kuepuka kupandikiza  chuki kwa chombo ama mwanahabari mwenzetu kwani iwapo  tutafanya  hivyo ni  sawa na kuivua nguo taaluma  yetu wenyewe .

Mungu  ibariki Tanzania ,Mungu ibariki tasnia  hii ya habari nchini
Amina
MWISHO 
      imetolewa na Francis Godwin 
Katibu mtendaji  chama cha  waandishi wa habari mkoa wa Iringa (IPC)
Tarehe 5/6/2014

Post a Comment

 
Top