GuidePedia

0


WAKULIMA wilayani Kyela mkoani Mbeya wametakiwa kuacha kulima kilimo cha mazoea na badala yake walime kilimo cha kisasa chenye tija ili wavune mazao mengi yatakayowaondoa katika wimbi la umasikini.

Kauli hiyo imetolewa na aliyekuwa  Mbunge wa Kyela na mkuu wa mkoa wa Mbeya mstaafu John Mwakipesile alipotembelewa na waandishi wa habari shambani kwake kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili wakulima.

Mwakipesile amesema kinachosababisha wakulima kuvuna mazao kidogo ni kutokana na kulima kilimo cha kizamani na upatikanaji duni wa pembejeo za kilimo hasa mbolea za Ruzuku zinazotolewa na serikali kupitia mawakala wao

“Serikali kuu imekuwa ikitumia mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kununua mbolea kwa ajili ya kuwasaidia wakulima lakini tatizo lipo kwenye halmashauri za wilaya ambazo zimeshindwa kuwachukulia hatua watendaji na wenyeviti wanao chakachua mbolea hizo kwa kuandika majina hewa badala ya majina halali ya wakulima” alisema Mwakipesile.

Hata hivyo mwakipesile amesema kama hali itaendelea kuwa hivyo mkulima ataendelea kuteseka kwa kutonufaika na kilimo huku viongozi wa serikali za mitaa na maafisa watendaji wakiendelea kunufaika pindi zoezi la mbolea linapoanza.

                         

                          Na, Ibrahim Yassin Kyela


Post a Comment

 
Top