GuidePedia

0

Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Iringa, John Ndumbaro (kushoto) ambaye ni Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK) katika picha ya maktaba yetu inayomuonesha alipokuwa akikabidhiwa Sh Milioni 6 kutoka kwa aliyekuwa Meneja wa Benki ya Posta Tawi la Iringa, Nabwike Mwakajila baada ya kushinda droo ya promosheni ya Shiriki, Shinda, Jiwezeshe iliyoendeshwa mwaka 2010 na benki hiyo
SIKU chache baada ya Bunge Maalumu la Katiba (BMK) kupokea rasimu ya Katiba Mpya iliyopendekezwa, mmoja wa wajumbe wa bunge hilo anayetoka kundi la 201, John Ndumbaro ameibukia mjini hapa na kutaka vipengele kadhaa vifanyiwe marekebisho.

Ndumbaro anayetokea mjini Iringa akiwakilisha kundi la walemavu alisema jana kwamba walemavu wanahitaji kupata nafasi zaidi ya ile inayopendekezwa katika bunge.

“Tume ya Warioba ilitenga nafasi tano za wabunge wenye ulemavu kati ya wabunge 75 ambazo ni sawa na asilimia saba,” alisema.

Alisema pamoja na kwamba mfumo unaopendekezwa sasa unataka kuwepo kwa wabunge 360, nafasi za wabunge wawakilishi wa watu wenye ulemavu zimependekezwa ziwe tani ambazo ni sawa na asilimia moja.

Ndumbaro alisema kuna haja nafasi hizo zikaongezwa kutoka asilimia moja hadi tano ili watu wenye ulemavu wawe na idadi ya kuridhisha ya wawakilishi watakaowasemea mambo yao katika bunge.

Akiipongeza kamati ya uandishi wa katiba kwa kazi nzuri iliyofanya aliitaka iangalie mambo mengine mengi kwa uzito unaostahili kama ilivyojadiliwa kwenye kamati mbalimbali na ndani ya bunge hilo.

“Mambo hayo tumeyajadili kwa kina ndani ya mjadala wa bunge lakini hayajapewa uzito katika rasimu zote,” alisema.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kupewa nguvu ya kikatiba ili wala rushwa wakubwa na wadogo kwa pamoja waweze kuchukuliwa hatua kali zitakazosaidia kukomesha kabisa suala hilo.

Lingine lililotajwa na Ndumbaro ni suala la michezo analotaka liwe la kikatiba kwani ni nyenzo muhimu katika kujenga umoja, amani, mshikamano, upendo na utulivu.

“Lakini pia michezo ni ajira inayoweza kuondoa malalamiko ya vijana wengi kukosa kazi. Ili suala hili liwe la kipaumbele ni lazima liwe la Kikatiba,” alisema.

Post a Comment

 
Top